
Idadi kubwa ya wafanyabiashara mjini Kitale imechangia kuwepo kwa msongamano katika soko hilo la Kitale. Msongamano huo, umesababishwa na ujenzi wa barabara kuu inayoelekea nchini uganda pamoja na shirika la reli kuwafurusha wafanyabiashara hao kutoka kwenye ardhi yao.
“Njia ya kujipatia riziki ipo kwenye biashara. Tunahitaji vijana wadogo ambao wana ubunifu, wawe wabunifu katika kufanya biashara. Wajihusishe na shughuli za biashara ili waweze kupata fedha za kujikimu kwenye maisha,” mwenyekiti wa wafanyabiashara Trans Nzoia, Martin Waliaula alisema.
Serikali kuu na ile ya kaunti, inahimizwa kutatua suala hilo haraka iwezekanavyo, ili kuwasaidia wafanyabiashara hao na mahali pa kuendeleza shughuli zao za uuzaji wa bidhaa.
“Tunahusisha serikali kuu ili iweze kutuongezea pesa ya kupanua ununuzi wa shamba la reli na pia tunatarajia gavana wa kaunti hii kuweka mikakati ya kupata shamba la ekari moja kwenye shamba lile la gereza,” waziri wa biashara Trans Nzoia, Sternley Kirui alielezea.
Chama cha wafanyabiashara katika kaunti hiyo, kilitoa takwimu kwa kupungua kwa wafanyabiashara kwenye soko hilo, rai ikiwa ni kuwasaidia wafanyabiashara hao ili waweze kupata mazingira mazuri ya kuboresha biashara zao.
“Tunataka kuzindua masoko ya kisasa ambayo yanatumia nafasi kidogo ya ujenzi kwa kukimu wafanyabiashara wengi. Ujenzi huo utakuwa mfano wa ghorofa ambapo wafanyabiashara wengi watafanya biashara zao kwa pamoja. Tukipata ekari kumi tunatumai mpango huo utatimia ikiangaziwa kuwa wafanyabiashara wa jua kali wamesongamana zaidi,” Sternley Kirui aliongezea.
Hata hivyo, chama hicho kimetoa wito kwa serikali ya Trans Nzoia kuweka mikakati ya ujenzi wa soko mashinani ili kupunguza msongamano unaoshuhudiwa mjini kitale.