
Akiamuru kuondolewa kwa kesi hiyo, hakimu Victor Wakumile alisema kuwa hakuna ushahidi wa msingi wa kuendeleza kesi hiyo ya ufisadi iliyomhusisha naibu wa rais Rigathi Gachagua na wengine saba kwa tuhuma za kupora shilingi bilioni saba.
Hata hivyo hakimu huyo alisema kuwa washtakiwa wanaweza kukamatwa na kushtakiwa tena iwapo ushahidi dhidi yao utapatikana. Uchunguzi bado unaendelea ili kupata ushahidi wa msingi wa kurudisha mashtaka ya washukiwa hao.
“Washtakiwa hao wanaonywa na kujuzwa kuwa wanaweza wakakamatwa tena kwa madai haya haya ya ufisadi,” hakimu victor wakumile alitoa onyo hilo baada ya kuondoa kesi hiyo kwa kukosa ushahidi wa msingi.
Hilo likijiri baada ya upande wa mashtaka kuomba mahakama kuondoa kesi hiyo, ukidadisi kuwa hakuna ushahidi wa msingi ikizingatiwa kuwa bado uchunguzi unaendelea. Akizungumza baada ya kuondolewa kwa kesi hiyo kwenye mahakama hiyo ya milimani, seneta wa Nyeri, Wahome Wamatinga amesema kuwa maafisa wa polisi kwenye idara ya usalama hawawezi tumiwa vibaya na serikali kuwakandamiza viongozi na wananchi kutokana na uhuru wa kauli mbalimbali wanazozitoa.
“Serikali iliyopo inafaa kuhakikisha kuwa inawahakikishia wakenya kuwa jambo kama hili halitendeki tena. Polisi hawatatumiwa kutekeleza vitendo vibaya kwa kulazimishwa na maafisa kwenye serikali kuwakandamiza wakenya kwa kauli mbalimbali wanazotoa. Hakikishi letu ambao tupo kwenye mabunge ya kitaifa ni kukabiliana na suala hilo,” seneta wa Nyeri, Wahome Wamatinga alisema.
Awali upande wa mashtaka ulisema kuwa hakukuwa na ushahidi wa kuendeleza kesi hiyo ila baadaye mpelelezi mkuu wa dci, obadiah kuria alipendekeza kesi hiyo iendelezwe akisema kuwa aliamurishwa hivyo na aliyekuwa mkuu wa idara ya DCI George Kinoti aliyejiuzu punde tu rais william ruto alipoingia mamlakani.
Afisa huyo wa upepelezi alikuwa na wakati mgumu mahakamani kujitetea na madai hayo aliyoitumia mahakama hiyo kupitia hati kiapo, akiilezea mahakama kuwa iendeleze kesi hiyo baada ya kushurutishwa na mkubwa wake, aliyekuwa mkuu wa DCI George Kinoti.
Na James Chacha