
Baada ya kuapishwa na kuingia ofisini wiki iliyopita, Waziri wa Utumishi wa Umma, Jinsia na hatua Aisha Jumwa, alisema kuwa mishahara ya wafanyakazi wote wa utumishi wa umma itapitiwa hivi karibuni ili kuongeza uadilifu wao. Alikuwa katika ziara yake ya Kenya School of Government (KSG) Mombasa. Hii ilikuwa ziara ya kwanza rasmi kwake katika nafasi yake kama Waziri mjini Mombasa na mkoa wa Pwani.
“Na tutashirikiana na wajumbe wetu, tutawapatia mwelekeo na mwongozo wa ni vipi wanaweza kujenga huduma centres katika mashinani kabisa alafu zile ‘platform’ na huduma ambazo serikali tumeshirikiana wizara kadhaa kuleta huduma kwa wananchi zikaweze kuwa katika mashinani, hayo ndo malengo ya huduma.” Waziri Aisha Jumwa alisema.

Kwa sasa kuna vituo vya huduma za serikali ama Huduma Centres arubaini na moja kote nchini. Waziri Aisha Jumwa alisema kwamba mikakati imeanza kupangwa ili kuongeza idadi ya vituo hivyo hadi kwa maeneo bunge. Ni wazi kwamba vituo hivyo hukua tu katika miji mikubwa na hivyo huwa ngumu kwa wananchi wengine kufikia vituo hivyo.
“Huduma Kenya Program’ imefanya maajabu na nimefurahia sana na ndio maana nikasema kwamba siku mia moja zinazokuja katika ofisi, mimi Pamoja na hiki kikundi chetu cha huduma tuko na mipango ambayo tutaenda kutekeleza na ya kwanza ni ile ambayo nilitangaza kwamba tumeongeza muda wa kuwahudumia wananchi kutoka saa moja asubuhi mpaka saa moja jioni.
Waziri huyo pia amesema serikali ina mpango wa kuongeza utendakazi wa wafanyakazi wa Utumishi wa umma na kwamba hii itaafikiwa kwa kuwahamasisha. Pia alisema kwamba kuna upungufu wa wafanyakazi hao, kwamba takriban watu laki tisa wanahudumia watu milioni arubaini na tisa.
“Uhaba wa wafanyakazi wa utumishi wa umma upo, tuko na wafanyakazi mia tisa elfu, chini ya milioni moja na wanawahudumia wananchi takriban milioni hamsini. Hii inamaanisha kwamba wafanyakazi wanafinyika sana kwa kufanya kazi nyingi kupita inavyotarajiwa.”
Alimalizia akisema atahakikisha kuwa wakenya wanapokea huduma bora zaidi jinsi inavyotakikana. Hivyo basi kwa kuhakikisha kwamba wakenya wanapokea huduma iliyo bora, wafanyakazi wa kutoa huduma hizo ndio wanapaswa kushughulikiwa na kuwapa motisha ya kuwahudumia wakenya jinsi inavyotakikana.
Na Calvin Angatia