Wanaboda boda Bungoma walalamikia hali ngumu huku wakimtaka Rais atekeleze aliyoahidi

0
9

Waendeshaji bodaboda kutoka Nalondo Magharibi, Kabuchai, Kaunti ya Bungoma hii leo wamejieleza kuhusiana na masuala yanayowahusu. Kwanza, walilalamikia gharama ya maisha nchini. Walisema kwamba serikali ya Rais William Ruto iliahidi kwamba wakiingia serikalini watapunguza gharama ya maisha lakini mpaka sasa ni ndoto.

Walilalamikia bei ya mafuta ambayo imepanda sana. Waendeshaji bodaboda hutegemea mafuta kutekeleza kazi yao ya kila siku na hivyo bei ya mafuta ikipanda inawatatiza sana na wanapata ugumu. Rais William Ruto alisema kwamba akiingia serikalini atapunguza bei ya mafuta lakini pindi alipoingia tu, bei ikapanda maradufu.

Mmoja wao alisema kwamba Rais Ruto alisema kwamba rais mstaafu asidanganye wakenya kwamba vita vya Ukraine na Urusi ndivyo vinavyofanya maisha kupanda. Sasa inasemekana kwamba pia Rais Ruto anaambia wananchi kwamba ni vita hiyo ndiyo chanzo cha gharama ya maisha kupanda.

Pia walilalamikia uongozi ambapo viongozi wanaahidi mengi lakini kutekeleza ni ngumu. Walitumia mfano wa mwakilishi wodi wao (MCA) ambaye aliwaagiza atawaundia barabara zote za eneo lao. Ni wazi kwamba ameanzisha shughuli za kuchimba barabara na haweki ‘murram’ ambapo sasa inatatiza usafiri hasa watu wa bodaboda ambapo unapata kwamba pikipiki inateleza sana.
“Wakati MCA wangu wa West Nalondo (Polycarp Wandabusi) alikuwa anafanya kampeni, alisema kwamba jambo la kwanza akiingia atahakikisha ya kwamba njia yoyote inayopatikana West Nalondo atatengeneza. Kuna mahali nilitembea nikaona ameanza kutengeneza hiyo njia lakini shida ni kwamba yeye anachimba tu barabara lakini haweki ‘Murram’. Sasa mvua ikinyesha, sisi kama wanabodaboda tunaumia sana.” Eliud Sifuna, mmoja wao alisema.
“Pia MP wetu akifanya kampeni zake aliahidi kwamba atasimama na sisi watu wa chini kama wa bodaboda na wafanyibiashara wadogo wadogo kama mama mboga. Tangu aingie kuwa mbunge wetu hajaweza kutusaidia.” Eliud Sifuna aliendelea.

Jambo lingine muhimu walilotaka lishughulikiwe ni kwamba wananchi katika kaunti ya Bungoma waachwe pekee kuamua kuhusu kiti cha Useneta kati ya UDA na FORD Kenya kufuatia mzozano baina yao kwa sababu ni wananchi wanaoumia. Haya yanajiri baada ya Seneta wa Bungoma Moses Wetangula kuidhinishwa kuwa spika wa Bunge la Kitaifa na kuacha kiti hicho wazi.

Mwisho, walitaka wanasiasa wakome kujihusisha na masuala yao ya kibinafsi na wanahitaji kuruhusiwa kuchagua mwakilishi wao ambaye atakuwa akiwasaidia kupata fedha za serikali kama vile hazina ya ‘Hustlers.’

John Wekesa, mwanaharakati wa Shirika la Kituo cha Haki za Kibinadamu alisema kuwa atasimama na wanabodaboda hata kama itabidi kwenda mahakamani. Alisema kwamba wanabodaboda wasiogope kutekelesha shughuli zao za kila siku. Pia alisema kwamba wanasiasa waache kujihusisha na masuala ya waendeshaji bodaboda.
“Mimi kama mtetezi wa haki za kibinadamu, nitawatetea hawa watu wa bodaboda hata kama ni kuenda kortini niko tayari kwenda kutaka kujua kwa nini polisi wanaingilia uchaguzi wao na kwa nini wanasiasa wanaingilia kazi zao

Na Calvin Angatia

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here