Pigo kwa wafugaji Kajiado; athari za ukame zaathiri soko la mifugo

0
58

Idadi ndogo ya mifugo wanauzwa katika soko la mifugo, idadi hiyo imepungua kutokana na hali ya ukame inayoendelea kushuhudiwa katika kaunti ya Kajiado. Wafugaji kwenye kaunti hiyo wanategemea
uuzaji wa mifugo kama nguzo muhimu ya kibiashara, kwa sasa wanalalamikia hali ya ukame ambayo
imezorotesha ufugaji.

“Nilikuwa na ng’ombe ishirini, kumi wamekufa na kumi ambao wamebaki nimewaleta niwauze hapa
sokoni. Nitawauza wote kwa sababu ya hali mbaya ya kiangazi inayoendelea kushuhudiwa katika
maeneo haya,” Ephuntus Parmasaen, mfugaji Kajiado alisema.

Bei ya uuzaji wa mifugo imepungua kutokana na mifugo kukosa lishe bora na maji. Ng’ombe
waliokuwa wakiuzwa bei kati ya elfu 70 na 50, kwa sasa wanauzwa kwa elfu 10. Wale ambao
wameathirika kabisa na uhaba wa lishe na maji kutokana na kiangazi huuzwa kwa bei ya chini zaidi.
Bei hiyo ya chini ambayo imeshuhudiwa kwenye soko la mifugo imesababishwa na janga la ukame
ambalo linaendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini. Wafugaji hao katika kaunti ya
kajiado wamelazimika kuuza mifugo wao ili wasipate hasara zaidi ya wao kufa.

‘Tunapoangalia hivi sasa, ng’ombe wanapungua kwa idadi kwa sababu ya ukame. Jambo hilo
linahatarisha maisha ya jamii yetu ya maasai kwa sababu tunategemea ufugaji wa mifugo,’ Joshua
Saigilu, mwakilishi wadi Ilodokilani alisema.

Wafugaji hao wamelalamikia kuwa bei wanayouza mifugo wao haitoshi kulipa karo ya shule.
Wengine wameshindwa kabisa kuuza mifugo yao sokoni. ‘Ng’ombe ndio hawa nimeshindwa
kuwauza, hakuna mtu anataka kuwanunua. Nimejaribu kuwauza haiwezekani na wengine wanakufa’,
Ndubuko Ole Nkoyo, mfugaji Kajiado aliteta.

Baadhi yao wamesema kuwa uchumi umekuwa mbaya sana, wameteta wakisema kuwa bei ya
bidhaa katika maduka imeongezek kwani hawawezi pata pesa ya kutosha ya kukimu familia zao,
kutokana na uhaba wa pesa ambao unatokana na uuzaji wa mifugo wao.

Mamlaka ya ukame nchi, ilitoa ripoti kuwa asilimia 50 ya mifugo wameangamia kutokana na hali ya
ukame inayoendelea kushuhudiwa nchini. Hata hivyo wafugaji katika kaunti hiyo ya kajiado wameirai
serikali kuwasaidia kwa njia mbalimbali ili waweze kusaidika kutokana na hali hiyo ngumu.

“Serikali ingetusaidia kuchimba visima vya maji ili watu wafanye ukulima kama inawezekana. Hili tu
ndilo tegemeo tunalohitaji kutekelezewa kwa sasa. Tuna wasiwasi ukame ukizidi mpaka mwaka ujao
hatuwezi saidika,” mfugaji mmoja alisema.

Maeneo mengi nchini yameweza kuathirika kutokana na hali ya kiangazi inayoendelea kushuhudiwa
katika maeneo hayo. Mifugo wameweza kushuhudiwa wakifa kutoka na uhaba wa lishe bora na maji.
Kaunti ya mandera ni mojawapo ya maeneo ambayo yamekumbwa na mifugo kufa kutokana na
ukame. Licha ya serikali kutoa misaada kwa maeneo athirika bado kungali na changamoto ya ukame
kwa sababu suluhisho la kudumu halipo.

Na James Chacha

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here