
Wakulima wa kahawa kule Nyeri wamelalamikia hali ya kiangazi inayoendelea eneo hilo huku
mimea yao ya kahawa ikiendelea kunyauka kila uchao. Wengi wamedai kwamba wanategemea
kahawa hiyo ili wapate mapato ya kukidhi maisha yao.
Eliud Nderitu, mzee wa miaka 65 ambaye ni mmoja wa wakulima hao wa eneo la Kiganjo
amesema kwamba maisha yake yote amekuwa mkulima wa kahawa. Pia anasema watoto wake
wote ambao wamemaliza masomo yao sasa wamenufaika pakubwa kupitia mapato ya kahawa.
Amepanda kahawa kwenye shamba lake la ekari tatu na kunyauka huko kulikuwa dhahiri sana.
Anaeleza hofu yake.
“Hii jua imewaka sana, imekuwa tangu mwaka wa 2019 mfululizo. Imeleta shida ya kwamba ile
shamba ambayo unavuna kahawa mingi, sasa huvuni, kwa sababu jua likiingia hakuna la
kufanya na ile kitu sisi tunategemea hapa ni kahawa.” Eliud Nderitu.
Anaeleza kwamba msimu wa mvua haujaonekana kwa miaka mitatu sasa na ndio chanzo cha
mikahawa kuanza kukauka. Anasema kwamba suala la serikali kuwekeza kwa uzalishaji
haliwezekani bila mvua.
“Mwaka huu katika msimu huu nilikuwa na 310 kilos, nikaweka shamba yangu mbolea nikavuna
kilo elfu nne.”
“Tumejenga matanki ya kuweka maji, na tukiweka maji hakutakuwa na njaa tena eneo hili.”
Godfrey Kagondu pia kwa upande wake anasema kwamba shamba lake pia limeathirika na
kiangazi na suala hilo lisipoangaziwa, watapata hasara kubwa mno. Anaeleza kwamba wakulima
wengi waliweka pesa mingi sana kununua mbolea lakini sasa ikakuwa hasara kwa sababu bila
maji mbolea inakuwa haina maana sana.
Wote wanaitaka serikali iingilie kati kuwaokoa ili wasivune hasara tupu. Wanaelezea pia serikali
yafaa yasaidie kila aina ya mkulima, awe wa kahawa, mahindi, au ng’ombe.
“Tunashangaa tukiona magari yakipita na mahindi kuelekea upande mwingine. Waache
kuangalia tu wakulima wa mahindi. Kila mtu tusaidiwe, kila mkulima asaidiwe kulingana na ile
kilimo ako nayo.” Godfrey.
Ni hali ambayo inatishia mavuno ya wakulima wengi kule nyeri, wakitaka serikali na viungo
vingine kukamilisha miradi ya maji ambayo imekwama ili kuwaokoa kwenye hatari hiyo
ambayo itawaumiza.
Na Calvin Angatia