Athari za ukame zazidi Mandera, Gavana aitisha usaidizi zaidi.

0
44

Baada ya ripoti kutolewa kuwa zaidi ya wakazi laki tano katika kaunti ya mandera wanahangaika
kutokana na janga la ukame, athari zaidi ya mifugo kufa imeshuhudiwa. Mifugo zaidi ya milioni moja
wamekufa kutokana na ukame unaokabili kaunti ya Mandera.
Akizungumza katika ufunguzi wa bunge la kaunti ya mandera, gavana Mohammed Khalif amesema
kuwa misaada ya maji na chakula itatolewa ili kuwasaidia wakazi wa kaunti hiyo. Ukame katika
kaunti hiyo umefanya wakazi wasipate mahitaji maalum yakiwemo; chakula, maji na pia njia za
kupata pesa.
Amesema kuwa kutakuwa na usambazaji wa chakula katika shule mbalimbali katika kaunti hiyo ili
kupunguza idadi ya wanafunzi wanaoacha shule kutokana na ukosefu wa maji na chakula.
Waathiriwa katika sehemu hizo hukumbwa kwa kiasi kikubwa na hii hupelekea wanafunzi kuacha
masomo.
‘Kuna haja ya kuchukua mikakati ya dharura, ikiwemo kusambaza maji kwenye shule na pia kutoa
misaada ya chakula kwa shule 41 ambazo wanafunzi huishi na kwa zaidi ya vituo 300 vya watoto
ambao hukosa mahitaji ya kimsingi katika kaunti yetu,’ gavana wa Mandera, Mohammed Khalif
alisema.
‘Tunairai serikali kuu na mashirika ya mazingira kutusaidia katika mikakati hiyo. Tukiendelea kupitia
ugumu huu, tunafaa kujua kuwa tunakumbwa na janga la ukame kutokana na mageuzi ya hali ya
anga. Kutotabirika kwa majira yanayoshuhudiwa katika kaunti hii, kumefanya ufugaji na ukulima
kuwa vigumu’, gavana aliongezea.
Watoto chini ya miaka mitano katika kaunti hiyo hukumbwa na tatizo la utapio mlo kwa kukosa lishe
bora. Hata hivyo serikali ya kaunti hiyo imepanga kuwekeza kilimo kando mwa mito ili kuimarisha
uzalishaji wa chakula, kukimu uhaba wa chakula unaoshuhudiwa.
Viongozi mbalimbali katika kaunti hiyo wamemuunga mkono gavana huyo wakisema kuwa yale
ambayo gavana aliyagusia yatawasaidia sana wakazi wa kaunti hiyo. Wamemhakikishia kuwa
watamsaidia kwa vyovyote, kwa lengo la kuwasaidia wakazi wa mandera dhidi ya matatizo
yanayoletwa na janga la ukame.
‘Mbinu za kujimu kwenye maisha, matatizo ya maji, elimu, chakula yamezungumziwa peupe kwenye
hotuba ya gavana. Haya, kama bunge la kaunti na viongozi waliochaguliwa kuongoza wananchi
yatatimizwa kufuatia ombi la gavana kwa lengo la sisi kumsaidia kutatua shida hizo’, mmoja wa
kiongozi katika bunge la kaunti alisema.
‘Mkutano ulikuwa wa haki, gavana ameongelea mambo mengi ya muhimu yakiwemo hali ya janga la
ukame na pia njia za kujizuia na janga hilo. Tunafurahia ameleta mipango mbalimbali ambayo
itaidhinishwa kwenye serikali yake’, kiongozi mwingine wa bunge la kaunti hiyo aliongezea.
Mandera ikiwa miongoni mwa kaunti mbalimbali nchini zinazoendelea kushuhudia janga la ukame,
serikali za kaunti kutoka maeneo yanayokumbwa na ukame na serikali kuu zimeweka mikakati ya
kuwasaidia waathiriwa. Serikali kuu imekuwa ikitoa misaada ya chakula na maji katika maeneo hayo.
Mipango zaidi imewekwa kuhakikisha kuwa wanaokabiliwa na ukame wanatapa kusaidiwa kwa
haraka kabla ya madhara kuzidi.

Na James Chacha

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here