
Familia moja katika eneo la Thunguma eneo bunge la mji wa Nyeri, kaunti ya Nyeri inatoa wito
kwa Wakenya wenye nia njema kuwasaidia kuelewa ugonjwa wa ajabu katika familia ambao
umewashuhudia wakidhoofika kadri miaka inavyosonga. Ugonjwa huo unafanya miguu kulegea
na hivyo mtu anahitaji magongo au mkongojo kutembea.
Geoffrey Mwangi, Rose Nyawira, Charity Wamboi na Daniel Njuguna ndio walioathirika.
Walizaliwa wote wakiwa sawa lakini ikafika wakati miguu ikaanza kulegea na kukosa nguvu na
hivyo wakahitaji kutafuta vifaa vya kujishikilia wakitembea. Beatrice Maina ni rafiki wa karibu
wa familia hiyo na anelezea.
“Wote walikuwa wazima, lakini miaka ikizidi kuenda wanakuwa viwete. Lakini tunafikiria ni
maneno ya nyumbani kwa maana ni kama inarithiwa, kwa maana wote, hata watoto wao
wanazaliwa wakiwa wazuri lakini wanapofika wakati fulani wanakuwa viwete. Sasa mtu anakuja
hapa anawaangalia mpaka analia.” Beatrice Maina.
Familia hiyo inaishi maisha ya kubahatisha huku wakitelekezwa na wanakijiji wakiona kwamba
wao ni laana. Wenye nia njema tu ndio wanaokuja kuwasaidia mara kwa mara. Wanaishi nyumba
ambayo iko katika hali mbaya sana.
“Hakuna mtu ata mmoja kutoka katika familia anaweza kuja hapa kuwaangalia na kila mtu
anasema kuna shida. Lakini ni kujikakamua tu na kuona heri uwapee kitu, hata mtu anajinyima
lunch na kuleta.” Beatrice

Mfanyibiashara mmoja wa Nyeri aliwasaidia kwa kuwaletea vifaa vya samani ili angalau wapate
kuishi kama mtu yeyote yule wa kawaida. Alisema kwamba aliona tu ni heri awapatie viti vya
kukalia na hata pia kulalia kwa sababu muda mwingi wanatumia kuketi.
Familia hiyo wameomba kwamba mtu yeyote anayeweza kujua ugonjwa huo na jinsi ya kuutibu
ajitokeze aweze kuwasaidia kwa sababu wanaumia sana. Wanaowatakia mema pia wameomba
angalau kama kuna jinsi mtu yeyote anaweza kuwasaidia aweze kuingilia kati na pia serikali. Pia
wameomba nyumba yao ifanyiwe marekebisho ili waishi maisha mema.
“Kwa serikali tunajua kuna vitu vingi ambavyo wanapeana, hata kuna pesa zimetengwa
kuwasaidia watu kama hawa. Shida ni kwamba hakuna mtu wa kufuatilia.” Beatrice.
Na Calvin Angatia