
WAZIRI MTEULE WA ELIMU YUKO TAYARI AU LA?
Baada ya uteuzi wa mawaziri siku ya Jumanne na Rais William Ruto, kuna sekta mbalimbali ambazo zimeweza kuangaziwa sana kurejelea umuhimu au ukubwa wa sekta hizo. Sekta mojawapo iliyoongelewa ilikuwa sekta ya elimu. Rais alimteua Ezekiel Machogu kuwa Waziri
mpya wa elimu ambaye atamrithi Profesa George Magoha. Swali ni je, Waziri huyo mteule yuko tayari au la? Waziri ambaye anaondoka sasa Profesa George Magoha aliweza kuleta mambo mbalimbali
katika sekta ya elimu ikiwemo mfumo wa CBC ambao alifanya juu chini kuhakikisha mfumo huo umesimama imara. Aliupigia debe mfumo huo na hakutaka kusikia yeyote akipinga huku ikizingatiwa ukali wake.
Mfumo huo uliweza kuleta hisia mbalimbali huku wazazi wengi wakiukataa. Sio kila mzazi aliweza kupendezwa nao. Wengine walidai kwamba CBC ina gharama kubwa sana kwa kuwa kuna vitu kadha wa kadha ambavyo wanafunzi wanatakiwa kuwa navyo. Pia wengine walidai kwamba wanafunzi wanasumbua nyumbani kwa kuja na kuulizia vitu ambavyo vinakaa ni kama havina maana.
Baada ya uteuzi, wazazi wengi wametaka Waziri mpya ashughulikie suala la mfumo huo kwa makini sana. Waziri alisema kwamba yuko tayari iwapo ataidhinishwa na bunge.
“Ni doketi kubwa sana na wizara muhimu sana, na ninataka kuwahakikishia watu wa Kenya
kwamba kwa kweli nitaweza kufanya kazi bila kuchoka ili kuhakikisha kwamba tunaweza
kuboresha ubora wa elimu katika nchi yetu.” Alisema.
Kulingana na Dkt. John Mugo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Zizi Afrique, mfumo wa CBC una mianya ambayo inafaa kujazwa. Alisema kwamba kuna tu masuala mbalimbali ambayo yanafaa kurekebishwa na mfumo huo utakuwa bora.
“Suala la wanafunzi wa gredi ya sita kuenda shule ya sekondari ni suala ambalo halina msingi. Wanafunzi hawa ni wachanga sana na pia kuna mikasa mbalimbali ya shule ya upili kama vile kuchoma shule, na hivyo shule ya upili ya kwanza haina maana.” Alisema.
“Kuna maamuzi ya dharura yanatakiwa kufanyika, kwa mfano kosa la kuleta mitihani mingi ya
kuchagua majibu hadi darasa la sita, ni ya nini? Kwa sababu tuna mpito wa asilimia mia moja
kutoka darasa la sita hadi saba, kwa nini tunahitaji mtihani?” Aliongeza.
Pia aliongeza kwamba suala la NEMIS linafaa pia kushughulikiwa ili iwe bora au ya kufaa
kusanya data.
“Masuala ya data, tunajua kwamba Nemis imekuwa sasa hauwezi kujua tuna shule ngapi, kuna
wanafunzi wangapi katika kila kidato au darasa…” Daktari John Mugo alimalizia.
Katika mwaka wa 2021/2022, serikali ilitenga shilingi bilioni mia tano na tatu nukta tisa katika sekta ya elimu na haikutumiwa kikamilifu. Wakenya sasa wanasubiria iwapo waziri mpya ataweza kutumia kikamilifu fedha za wizara hiyo, ikizingatiwa kwamba ako na historia ya uongozi. Ameweza kuhudumu katika ofisi mbalimbali kama vile :
Elfu moja kenda mia sabini na sita – Mkuu wa wilaya
Elfu moja kenda mia themanini na tisa hadi elfu mbili na nane – Kamishna wa wilaya
Elfu mbili na nane – Alihudumu katika ofisi ya umma
Elfu mbili kumi na saba – Mbunge wa Nyabari Masaba
Tunasubiri tu aweze kuidhinishwa na bunge ili kuanza kutekeleza majukumu yake.
Na Calvin Angatia