
Wabunge wa muungano wa Azimio One Kenya walikutana tarehe kumi na sita Septemba katika
hoteli moja Machakos pamoja na viongozi wao wakiongozwa na Raila Amollo Odinga,
Martha Karua na Kalonzo Musyoka. Haja kuu ya mkutano huo ilikuwa ni kuzungumzia mikakati
ambayo watatumia kuendesha shughuli zao kama wapinzani. Raila Odinga alizungumzia tu
baadhi ya mikakati hizo.
Aidha, ilikuwa wazi kabisa kwamba katika mkutano huo, mwenyekiti wao ambaye ndiye sasa
rais mstaafu Uhuru Kenyatta hakuweza kuhudhuria. Ikumbukwe kwamba mkutano uliofanyika
tarehe saba Septemba katika Maasai Lodge, Kajiado aliweza kuhudhuria. Katika mkutano huo,
Uhuru Kenyatta alizungumzia mambo muhimu ikiwemo kwamba wabunge wa Azimio
wasikubali kununuliwa na wana Kenya Kwanza na pia akasema kwamba rais wake si mwingine
bali ni Raila Odinga.
Wadadisi wengi wamejiuliza maswali mengi sana. Itakuaje mwenyekiti wao kukosekana katika
mkutano huo wa Machakos? Labda jawabu sahihi ni kuwa baada ya rais mstaafu Uhuru Kenyatta
kupewa jukumu la au kazi ya kidiplomasia na rais William Ruto, hakutaka kujihusisha kwa
ukaribu na mikutano yoyote ya kisiasa, au hata labda alikuwa na mambo ya kibinafsi ya
kushughulikia. Kiini cha kukosa mkutano huo bado hakijaafikiwa.
Katika mkutano wa Machakos, baadhi ya mambo yaliyozungumziwa yalikuwa ni haja ya umoja
wa Azimio na wabunge wasikubali kushawishiwa na kununuliwa na Kenya Kwanza.
Kilichobakia sasa ni kusubiria kujua kama rais mstaafu Uhuru Kenyatta ataendelea kuwa
mwenyekiti wa Azimio au atajitoa katika mambo ya kisiasa.
Na Calvin Angatia.