
Magavana kutoka kaunti zote nchini waliandaa kongamano la siku tatu katika kaunti ya Mombasa. Lengo la mkutano huo likiwa ni kuanzisha baraza la magavana baada ya kuapishwa kwao.
Kulingana na magavana hao ,Serikali nyingi za kaunti zinang’ang’ana na bili kubwa ya mishahara, wakati awamu ya tatu ya ugatuzi inapoanza. Katika Siku ya pili ya mkutano huo, magavana walielewana kupunguza idadi ya wafanyikazi huku wakielezea kuwa idadi kubwa ya wafanyikazi imesababisha malipo makubwa ya mishahara ambazo kaunti nyingi zinakabiliwa nazo.
Tume ya EACC, hapo awali ilikuwa imewaonya magavana dhidi ya kuwafuta kazi wafanyikazi wa kaunti bila kufuata utaratibu ulio sahihi. Tume hiyo pia iliongeza kuwa magavana wa kaunti watawajibika kwa hasara yoyote ya pesa kutokana na kufutwa kazi kwa wafanyikazi hao.
Wakuu wa mkoa wameshikilia kuwa wanafahamu madhara yake na kila kitu kitafanyika kwa mujibu wa sheria. Vilevile wameshikilia kwamba hawataruhusu wafanyakazi hewa almaharafu kama ghost workers kwani watafanya ukaguzi wa bili kabla ya kulipwa. Bili zinazosubiri kukamilika zinaongezeka hadi mabilioni ya pesa. Hii ni baada ya gavana wa kaunti ya kisii Simba Arati kuwafuta kazi wafanyakazi mia nane sitini na mmoja.
Magavana hao wanataka serikali ya rais Wiliam Ruto kusambaza kikamilifu baadhi ya majukumu ambayo wanadai bado yamo katika serikali ya kitaifa.
Na Emmaculate Wamalwa