
Baraza la kitaifa la mitihani (KNEC) limetangaza kuwa tovuti ya kutathmini wanafunzi wa daraja au gredi ya sita itafunguliwa kati ya tarehe kumi na tano na thelathini Agosti mwaka huu, kuwaruhusu watahiniwa kuchagua shule za upili za chini au junior secondary, ambazo wangependa kujiunga nazo.
Wanafunzi milioni moja nukta mbili saba watafuzu kutoka shule za msingi, kujiunga na shule za secondari ya chini januari, mwaka ujao.
Mtihani wa kitaifa wa daraja la sita umeratibiwa kufanyika kuanzia tarehe ishirini na nane hadi thelathini Novemba mwaka huu. Mtihani huo utabeba asilimia arubaini ya alama, huku asilimia nyingine sitini ikigawanywa kati ya daraja la nne, tano na sita, kila daraja kati ya matatu hayo likibeba asilimia ishirini kwa mitihani inayotofautiana katika shule nchini.
Kundi la kwanza chini ya mtaala wa umilisi wa elimu (CBC) litatathminiwa katika masomo matano, yakiwemo hisabati, kiingereza, kiswahili au lugha ya ishara, somo la jamii, sayansi pia ikiwemo.
Wakati uo huo, katibu mkuu wa idara ya masomo ya kimsingi daktari Julias Juan, ameonekana kukubaliana na usemi wa wahenga kuwa, elimu bila amali, ni kama nta bila asali, akiwakosoa walimu wanaolemaza utekelezwaji wa mtaala wa umilisi wa elimu.
Wanafunzi milioni moja nukta mbili nne, wataufanya mtihani wa darasa la nane ,mwishoni mwa mwaka huu, kujiunga na shule za upili chini ya mtaala wa 8-4-4.. J.m,